Jina " Karagwe " kutokana na simulizi za wazee wetu mbali mbali na watafiti wa historia ya Karagwe kama ( Katoke 1975; 162) inaelezwa kwamba jina hili linatokana na kilima (angalia kielelezo hapa chini) kinachopatikana Kusini Magharibi ya Makao makuu ya wilaya ya Karagwe ,kwenye kijiji cha Kandegesho ,kata ya Nyakakika ambacho mtawala ( Omukama ) wa kwanza alifanya kafara ya kwanza. Taarifa zilizopo mtawala huyo alijulikana kwa jina la Nono ya Malija kutoka ukoo wa Basiita. Na kwamba kumbukumbu hii ya "Karagwe ka Nono "inatokana na ukweli kuwa Nono alikuwa mtawala wa mwisho wa wenyeji asilia kabla ya kuondolewa madarakani na Omukama Ruhinda mtoto wa Wamara. Inasemekana kwamba Nono aliondolewa kwa ujanja bila ya misukosuko wala mapigano ya aina yoyote. Kwa kifupi hii ndio kumbukumbu yake na chimbuko la historia ya jina Karagwe.
Wilaya ya Karagwe ni kati ya Wilaya saba (7) za Mkoa wa Kagera. Wilaya inapakana na Wilaya ya Kyerwa upande wa Kaskazini, Nchi ya Rwanda upande wa Kusini Magharibi, Wilaya ya Ngara upande wa Kusini na Wilaya za Missenyi, Bukoba Vijijini na Muleba upande wa Mashariki.
Wilaya ipo kilomita 105 kutoka Manispaa ya Bukoba –Makao makuu ya Mkoa wa Kagera. Wilaya inapatikana kati ya nyuzi 1o na 2o, 20' Kusini Latitudo 30o hadi 38,30 Mashariki Longitudo. Mwinuko wa ardhi kutoka usawa wa bahari ni mita 1,500 hadi mita 1,800. Hali ya hewa kwa ujumla ni joto la wastani wa degree 26oC. Mvua zinanyesha kwa wastani wa mm 1,040 hadi 1,200 kwa mwaka, kati ya mwezi Septemba na Januari na kati ya mwezi Machi na mwezi Mei.
Wilaya ya Karagwe ina eneo la kilomita za mraba 4,500 kati ya hizo kilomita za mraba 4,342 ni eneo la nchi kavu na kilomita za mraba 158 ni eneo la maji. Eneo linalofaa kwa kilimo ni Hekta 153,540 na eneo linalolimwa ni Hekta 82,808.5 sawa na asilimia 53.9.
Maeneo ya Utawala yamebadilika kutoka Tarafa 4, Kata 28, Vijiji 109 na Vitongoji 1,162 mwaka 2005 hadi Tarafa 5, Kata 23, Vijiji 77 na Vitongoji 629 mwaka 2014. Vitongoji 594 vipo katika Halmashauri ya Wilaya na vitongoji 35 vipo katika Mamlaka ya mji mdogo.
Waheshimiwa Madiwani wa kuchaguliwa wapo 23 na Waheshimiwa Madiwani Wanawake Viti maalum 7.
Kulingana na Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, Wilaya ya Karagwe ilikuwa na jumla ya watu wapato 332, 020. Kati ya hao 163,864 (wanaume) na 168,156 (wanawake), ambapo ongezeko la watu ni asilimia 2.9 kwa mwaka.
Maoteo ya watu kwa mwaka 2015 ni kuwa Wilaya ilikuwa na watu 351,555. Kati ya hao, wanawake ni 178,050 na wanaume ni 173,505. Aidha idadi ya kaya nayo imeongezeka toka kaya 72,836 mwaka 2012 hadi kaya 76,425 mwaka 2015.
SHUGHULI ZA KIUCHUMI:
1. KILIMO, USHIRIKA NA UMWAGILIAJI:
Kilimo ni mojawapo ya shughuli za kiuchumi inayochangia wastani wa asilimia 70 ya pato la Halmashauri. Kaya zinazoshiriki katika shughuli za kilimo ni 61,351 kati ya kaya zote 76,425 za wilaya ya Karagwe. Eneo linalofaa kwa kilimo ni hekta 153,540 kati ya hekta 4,500,000 ya eneo lote la wilaya. Eneo linalofaa kwa kilimo cha Umwagiliaji ni hekta 4,500 Pia Wilaya inashirikiana na wadau mbalimbali waliopo wilayani katika kuendeleza sekta ya kilimo. Baadhi ya wadau hao ni ELCT, Karagwe Agribusiness, MAVUNO, CHEMA, WORLD VISION, MATUNDA MEMA, BISHESHE WINE, KARAGWE ESTATE LTD, RADIO KARAGWE, RADIO FADECO, LUKALE WINE, KDCU, Matunda MEMA, KADERES NA OLAM.
Aidha zipo SACCOS 31 zenye jumla ya wanachama 46,319 na Chama 1 kikuu cha Ushirika (KDCU) kinachojishughulisha na ununuzi wa mazao ya wakulima. Wilaya imeanzisha na kujenga mradi mmoja mkubwa wa Umwagiliaji (Mwisa Irrigation Scheme) wenye ukubwa wa Hekta 120. Uhamasishaji wa wananchi kulima mpunga na mbogamboga unaendelea. Mradi huu utaongeza kipato cha mkulima wa Karagwe na kupunguza umaskini.
2. UFUGAJI NA UVUVI:
Wilaya ya Karagwe ina hekta 140,000 zinazofaa na hutumika kwa shughuli za ufugaji. Sekta hii uchangia kwa zaidi ya 10% katika ajira ya wananchi na pato la kaya. Mifugo ambayo hufugwa ni pamoja na ng’ombe, mbuzi, kondoo, nguruwe, kuku, bata na sungura.
Shughuli za Uvuvi ufanyika katika maziwa madogo ya Burigi, Rwakajunju, Kamakala na mto Kagera. Wilaya inayo mabwawa ya kuchimbwa 67 kwa ajili ya ufugaji wa samaki. Uzalishaji wa samaki ni wastani wa kilo 33,000 kwa mwaka. Aina za samaki wanaozalishwa kwa wingi ni sato/ngege, kambale mamba, kambale mumi, furu, ningu, soga na domodomo.
3. VIWANDA NA BIASHARA:
Mji wa Kayanga na Omurushaka pamoja na miji midogo ya Kihanga, Nyakaiga, Rwambaizi, Nyaishozi, Chanyamisa, Nyabiyonza, Nyakabanga na Ihembe ni kati ya miji inayokua kibiashara na yenye mwingiliano mkubwa wa shughuli za kiuchumi na kijamii. Maeneo haya yanaendelea kuwekeza katika viwanda vya biashara kama vile viwanda vya kukoboa Kahawa, viwanda vya kusindika maziwa, asali, kusaga na kukoboa nafaka. Shughuli za uzalishaji zinaendelea kuimarika na kuongeza uzalishaji, kupanua ajira, kukuza biashara ya uuzaji na ununuzi wa mazao tarajiwa na hivyo kuongeza kipato na kukuza uchumi, kuboresha maisha ya jamii, kupunguza umaskini wa kipato na hivyo kuchochea kasi ya kuondoa umaskini.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.