HATI SAFI ISIWE BANGO LA KUTUPUMZISHA TUJITUME ZAIDI KUIDUMISHA - RC MWASSA.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Fatma Mwassa ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kuidumisha hati safi waliopewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kwa kuongeza uwajibikaji, ufanisi na kuzingatia utekelezaji wa Mapendekezo wanayopewa na Wakaguzi badala ya kuifanya kuwa bango la kupumzika.
RC Mwassa ameyasema hayo leo tarehe 17 Juni, 2025 katika ukumbi wa Halmashauri (Angaza) wakati akitoa pongezi za hati safi na salamu kwenye Mkutano wa Baraza Maalum la Madiwani lililokusudiwa kujadili hoja na maagizo ya CAG ya mwaka 2023/2024.
" Nawapongeza kwa kupata hati safi na kupunguza hoja za zamani lakini nawasihi tuweke maono ya kuondoa hoja zote kwasababu inawezekana. Tuzingatie utekelezaji wa mapendekezo ikiwemo kutumia mifumo ya tehama katika utendaji kazi, Ufuatiliaji na usimamizi wa miradi na huduma kwa ufanisi na kuongeza uwajibikaji" Alisema RC Mwassa.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Karagwe mhe.Julius Kalanga Laizer amesema kuwa Halmashauri inajitahidi kupunguza madeni ya zamani pia alitumia nafasi hiyo kusisitiza utengwaji wa bajeti ya kulipa madeni ili kufuta hoja zinazotokana na madeni.
Aidha, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe mhe. Wallance Mashanda amesema kuwa, Halmashauri inaendelea kushughulikia mapendekezo ya hoja zilizobaki na baadhi zitafungwa baada ya ukaguzi wa mwaka 2024/2025 kwasababu zilishafanyiwa utekelezaji pia amewapongeza Watumishi kuendelea kudumisha upatikanaji wa hati safi kwa kufanya kazi kwa kufuata kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma.
Kikao kilihitimishwa kwa wito kwa Watumishi katika masuala ya utumiaji mifumo kwenye manunuzi na taratibu nyingine zinazohitaji mifumo ya tehama, uombwaji wa fedha za miradi mapema ili miradi ianze mapema, pamoja na maandalizi ya mapema kwa ujio wa Mwenge wa Uhuru 2025.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.